Kupatwa kwa Mwezi
Kupatwa kwa Mwezi (kwa Kiingereza: lunar eclipse) ni badiliko la mwangaza na rangi ya Mwezi kwa muda. Kunatokea wakati wa Mwezi kupita katika kivuli cha Dunia ambako nuru ya Jua haifiki kwenye uso wa Mwezi moja kwa moja.[1] Mwezi unaangazwa na nuru inayoakisiwa na Dunia na kuwa na rangi nyekundu[2]. Kwa hiyo Mwezi huwa na nuru hafifu ukionekana mwekundu katika kipindi cha kupatwa. Badiliko hili linatokea tu wakati wa mwezi mpevu linaweza kudumu saa moja hadi nne. Baadaye Mwezi unatoka tena katika kivuli cha Dunia unaonekana kama mwezi mpevu wa kawaida.
Sababu ya kupatwa kwa Mwezi
Kupatwa kwa Mwezi kunasababishwa na kivuli cha Dunia kinachomwaga giza juu ya Mwezi wote kabisa au baadhi ya sehemu. Hali hii inatokea wakati Mwezi - Dunia na Jua vikiwa vimekaa katika mstari mmoja, ikiwa Dunia iko kati ya Jua na Mwezi. Hapo kivuli cha Dunia kinafunika Mwezi. Inatokea tu wakati wa mwezi mpevu. Hali hii ni kinyume cha kupatwa kwa Jua ambako Jua, Mwezi na Dunia vinakuwa pia katika mstari lakini hapo Mwezi uko kati ya Jua na Dunia na hivyo ni Mwezi unaosababisha giza kwenye uso wa Dunia pale ambako kivuli chake kinapita juu ya Dunia.
Tofauti kati ya aina za kivuli wakati wa kupatwa kwa Mwezi
Mara nyingi kupatwa kwa Mwezi si rahisi kutambulika kwa sababu si kupatwa kikamilifu. Hapo Mwezi unapita katika nusukivuli cha Dunia tu. Nusukivuli ni hali ambako sehemu ya nuru inazuiliwa lakini sehemu nyingine bado inafika. Tofauti ya uangavu si kubwa sana.
Hali ya tofauti inatokea kama Mwezi unapita kwenye kitovu cha kivuli cha Dunia. Hapa tofauti ya uangavu ni kubwa inaonekana kabisa. Mara nyingi kitovu cha kivuli kinafunika sehemu tu ya Mwezi na hapo tofauti inaonekana kwenye uso wa Mwezi jinsi tunavyouona.
Wakati Mwezi wote umeingia katika kiini cha kivuli bado unaonekana kidogo, mara nyingi huonyesha rangi nyekundu. Sababu yake ni kwamba nuru ya Jua inapita katika angahewa ya Dunia na kutawanywa. Kwa hiyo nuru ambayo bado inakisiwa na uso wa Mwezi si nuru inayofika moja kwa moja kutoka Jua bali sehemu ndogo ya nuru tu iliyotawanywa na angahewa ya Dunia. Hapo masafa ya mawimbi marefu hayatawanywi katika angahewa kirahisi kama masafa mafupi na ndiyo sababu ya rangi nyekundu.
Marudio
Kupatwa kwa Mwezi hutokea kila mwaka, angalau mara mbili hadi mara tano. Lakini mara nyingi mwezi hufunikwa baadhi ya sehemu tu.[3] Jumla ya marudio 12,063 ya kupatwa kwa Mwezi yamekadiriwa kwa kipindi cha miaka 5,000 kuanzia mwaka 1999 KK hadi 3000 BK.[4]
Angalia pia
Tanbihi
- ↑ "Kupatwa kwa Mwezi Tarehe 10-11 Januari 2020". Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. 10 Januari 2020.
- ↑ Kwa Kiingereza hali hii huitwa pia "Blood Moon"
- ↑ Matokeo ya kupatwa kwa Mwezi kati ya 2011 hadi 2020, tovuti ya NASA, iliangaliwa Julai 2012
- ↑ Periodicity of Lunar eclipses, tovuti ya NASA
Viungo vya nje
- "Lunar Eclipse Essentials": video from NASA
- Animated explanation of the mechanics of a lunar eclipse Archived 3 Juni 2013 at the Wayback Machine., University of South Wales
- U.S. Navy Lunar Eclipse Computer Archived 13 Agosti 2011 at the Wayback Machine.
- NASA Lunar Eclipse Page
- Search among the 12,064 lunar eclipses over five millennium and display interactive maps
- Lunar Eclipses for Beginners
- Tips on photographing the lunar eclipse from New York Institute of Photography Archived 14 Julai 2011 at the Wayback Machine.
- Lunar Eclipse 08 October 2014 katika YouTube
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kupatwa kwa Mwezi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |