Mti
Mti ni mmea mkubwa wa kudumu wenye shina la ubao.
Miti huishi miaka mingi; miti yenye umri mkubwa imejulikana kuwepo kwa miaka 4,800 huko Kalifornia. Kuna dalili za mti mmoja uliopimwa huko Uswidi kuwa na miaka zaidi ya 9,000.
Kwa jumla ugumu wa ubao na uzito wake hutegemea namna ya kukua kwa mti. Miti inayokua polepole huwa na ubao mgumu na mzito zaidi; miti inayokua harakaharaka huwa na ubao mwepesi na laini.
Ufafanuzi wa mti
Ufafanuzi wa kimataifa ni hivi:
"mti ni mmea wa ubao, kwa kawaida wenye shina moja tu, unakua hadi kimo cha angalau mita mbili. Kama kuna mashina mengi, moja lifikie unene wa sentimita tano kwa kina cha kifuani cha mtu".[1]
Muundo wa miti
Kwa kawaida mti huwa na
Shina
Unene na urefu wa shina unatofautisha mti na mimea mingine kama vichaka ambavyo vina shina ya ubao pia. Shina linainua majani ya mti kufikia kimo cha juu ya mimea mingine penye nuru ambayo ni chanzo cha lishe ya mti kwa njia ya usanisinuru. Ndani ya shina kuna seli zinazofanya kazi ya bomba na kufikisha maji hadi kilele cha matawi. Katikati ya shina ubao unakufa ni kama mfupa wa shina na kuongeza uimara wake. Gnada la nje huwa na seli zinazoendelea kujigawa na kuongeza unene.
Mti ukikatwa shina huonyesha mara nyingi duara au miviringo ambazo ni alama ya hatua za ukuaji wa mti. Kuonekana kwa duara hizi kunategemea mazingira ya mti; nje ya kanda ya tropiki kuna majira yanayosababisha vipindi vya kukua na vipindi vya kukaa kwa mti na hivyo duara mpya inajitokeza kila mwaka. Kwa hiyo mti wa aina hii unaruhusu kuona umri wake kwa kuhesabu tu idadi ya duara za shingoni.
Mizizi
Shina refu na zito linahitaji mizizi inayolingana. Mizizi huwa hasa na kazi mbili:
- inakusanya maji na lishe kwenye udongo na kuyapeleka shingoni
- ni mguu ya mti na kuushika kwenye ardhi
Miti inakuza mzizi kulingana na tabia za udongo. Penye udongo laini sana kama mchanga mti unahitaji mizizi pana inayoshikana udongo katika mazingira yake. Miti mingine inakuza hasa mzizi kama boriti.
Matawi
Matawi ni alama ya mti lakini kuna pia aina kadhaa zisizo na matawi; kwa mfano familia ya Arecaceae yenye miti kama mnazi, mchikichi au mtende hukuza majani makubwa moja kwa moja kutoka shina.
Majani
Majani yana kazi muhimu kwa mti si mapambo tu. Kuna hasa shughuli mbili
- usanisinuru yaani kutumia nguvu ya nuru ya jua kwa kujenga molekuli za glukosi (aina za sukari) kama lisha yake. Kwa mazingira yake mti unasafisha hewa kwa njia hii na kutoka oksijeni.
- ugemkaji yaani majani hugemka maji; kwa njia hii inawezesha usafiraji wa maji na lishe ndani ya mti.
Miti na ekolojia
Mwaka 2017 idadi ya spishi za miti zilizojulikana ilikuwa 60,065. Karibu nusu ya spishi hizo ni sehemu ya familia 10 za kibiolojia na asilimia 58 za spishi zinapatikana katika nchi moja tu[2].
Miti ni muhimu sana kwa ekolojia ya dunia kwa sababu
- miti hushika ardhi hasa milimani kwa mizizi yake. Hivyo inazuia mmomonyoko wa udongo.
- miti hutunza kiasi kikubwa cha maji na kwa njia hii hali ya hewa duniani; miti inapokea maji ya mvua na kuiacha polepole.
- miti inatunza ndani yake kiwango kikubwa cha hewa ya CO2 na kuiondoa hewani wakati wa kukua.
Tanbihi
- ↑ Ufafanuzi rasmi wa IUCN (International Union for Conservation of Nature and Natural Resources), kundi la Global Tree Specialist Group (GTSG) unasema: "a woody plant with usually a single stem growing to a height of at least two metres, or if multi-stemmed, then at least one vertical stem five centimetres in diameter at breast height."
- ↑ Linganisha Beech, Rivers, Oldfield, Smith: GlobalTreeSearch, angalia marejeo
Marejeo
- E. Beech, M. Rivers, S. Oldfield, and P. P. Smith, GlobalTreeSearch: The first complete global database of tree species and country distributions, tovuti ya Journal of Sustainable Forestry, ilitazamiwa Mei 2017
Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mti kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |