[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Maria Fransiska wa Madonda Matano

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sanamu ya Maria Fransiska wa Madonda Matano.

Maria Fransiska wa Madonda Matano (aliishi Napoli, Italia, tangu azaliwe tarehe 25 Machi 1715 hadi kufa tarehe 6 Oktoba 1791) alikuwa mwanamke ambaye watu wa Napoli walimheshimu hasa kutokana na maisha yake ya sala na upendo wake kwa Mungu na kwa maskini wa mitaa ya matabaka ya chini.

Aligusa watu pia kwa uvumilivu wake mkubwa mbele ya maumivu na mapingamizi mengi na ya mfululizo na kwa malipizi aliyoyafanya kwa wokovu wa wengine[1].

Kutokana na sifa zake, kisha kukusanya ushahidi wa maadili yake ya kishujaa na wa miujiza iliyozidi kutokea kwa maombezi yake, tarehe 12 Novemba 1843 alitangazwa na Papa Gregori XVI kuwa mwenye heri na tarehe 29 Juni 1867 alitangazwa na Papa Pius IX kuwa mtakatifu bikira.

Sikukuu yake huadhimishwa kila mwaka tarehe 6 Oktoba[2].

Anaombwa hasa na wanawake tasa wanaotamani kupata mtoto.

Anna Maria Rosa Gallo alizaliwa na Francesco Gallo na Barbara Basinsi katika mitaa ya jiji la Napoli. Tangu utotoni alionyesha imani kubwa, hata wakaanza kumuita "mtoto mtakatifu" kwa jinsi alivyofuata maisha ya sala na alivyovumilia ukali wa baba yake.

Wakati huo alianza kupata uongozi wa kiroho kwa padri Yohane Yosefu wa Msalaba, ambaye ni mtakatifu wa kwanza kutoka Italia wa urekebisho wa Ndugu Wadogo walioitwa Pekupeku. Yeye alitabiri kuwa binti huyo atakuwa mtakatifu kweli.

Alipofikia umri wa miaka 16, aliomba ruhusa ya kujiunga na Utawa wa Tatu wa Mt. Fransisko wa Asizi lakini akakataliwa, kwa sababu baba alikuwa amemuahidia kijana tajiri kwamba atamuoza kwake. Hata hivyo mnamo Septemba 1731 alimruhusu.

Anna Maria alipoweka ahadi yake ya kitawa tarehe 8 Septemba 1731, alijitwalia jina la Maria Fransiska wa Madonda Matano, kutokana na heshima yake kwa Mateso ya Yesu Kristo, Fransisko wa Asizi na Bikira Maria. Ingawa alivaa kanzu ya Kifransisko, aliendelea kuishi nyumbani kwa baba na kutendewa naye vibaya.

Alipofikia umri wa miaka 38 alikwenda pamoja na Mfransisko mwingine wa kike kuishi karibu na kiongozi wake wa kiroho, padri Giovanni Pessiri, alipobaki kwa miaka 38 hadi alipofariki akiwa na miaka 76 tarehe 6 Oktoba 1791.

Alikuwa na karama ya unabii, akitabiri mambo mbalimbali yaliyokuja kutokea kweli baadaye.

Pia alijaliwa madonda matakatifu na kupatwa na mateso makali kila Ijumaa na siku zote za Kwaresima.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.