Mabati
Mabati ni vipande bapa vya chuma vilivyofunikwa na ganda jembamba la zinki. Yanatumika kwa ujenzi, hasa kwa kufunika paa, lakini pia kwa shughuli nyingine kama kutengeneza kuta za majengo au kwa ajili ya magari. Zinki inazuia kutu isiharibu chuma.
Umbo la kawaida
Kuna aina mbalimbali za mabati. Umbo linalotumiwa mara nyingi ni bapa ikiwa na mabonde umbo la viwimbi. Umbo hilo linafanya bati kuwa imara zaidi: halikunjiki kirahisi kwenye mwelekeo wa mabonde yake lakini bado linaweza kuviringishwa.
Umbo hilo lilivumbuliwa huko Uingereza na hatimiliki ilitolewa mwaka 1829 kwa mhandisi Henry Robinson Palmer.[1]
Faida za ujenzi kwa mabati
Mabati ni mepesi na hubebwa kirahisi. Katika ujenzi faida yake ni gharama ndogo kwa sababu mabati yanafungwa juu ya maunzi ya ubao au feleji. Maunzi yanaweza kujengwa mepesi pia kwa sababu hayana kazi ya kubeba vitu vizito. Pia si gharama kubwa kupeleka vifaa hivyo vyepesi hadi mahali pa kujenga. Wafanyakazi wachache wanaweza kufunga mabati juu ya maunzi ya ndani. Yote hayo hupunguza gharama za ujenzi.
Hutumiwa kwa ajili ya majengo mbalimbali kama vile kuta na paa vya
- karakana na viwanda
- zizi la wanyama au ghala za vyakula
- gereji ya magari
- matangi ya maji
- nyumba rahisi za kuishi watu hasa katika mitaa ya vibanda
Hasara
Hayapendezi kwa ujenzi wa nyumba za watu lakini kutokana na gharama ndogo watu maskini wanayatumia mara nyingi. Hasara ya nyumba hizo ni ukosefu wa kinga dhidi ya joto na baridi kwa sababu metali ya mabati inapitisha joto na baridi haraka.
Si kifaa cha kudumu sana. Hali halisi zinki juu ya mabati hayawezi kuzuia chuma kushikwa na kutu. Hatari ni hasa mvua asidi au chumvi hewani katika maeneo karibu na bahari na katika mazingira hayo kutu inaonekana baada ya miaka michache. Mabati yanaweza kukingwa zaidi kwa kuyapakia rangi.
Aina nyingine za vifaa vinavyoitwa mabati
Umbo tofauti ni lile ya trapezi pachasawa ambalo ni imara zaidi.
Bapa kama mabati hutengenezwa pia kwa kutumia feleji au alumini; zinaweza kufunikwa kwa ganda la rangi au plastiki badala ya zinki au juu ya zinki. Kama bapa za plastiki zinapewa umbo la viwimbi wakati mwingine zinaitwa pia "mabati" na kutumiwa vile.
Umbo la bapa ya viwimbi hutengenezwa pia kwa saruji ya kuimarisha kwa kuiga mfano wa mabati.