[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Joseph Kabila

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Joseph Kabila.

Joseph Kabila Kabange (alizaliwa 4 Juni 1971) alikuwa rais wa nne wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Aliingia urais baada ya kifo cha baba yake Rais Laurent-Desiree Kabila aliyeuawa na wanajeshi tarehe 16 Januari 2001. Wanasiasa wengine walimteua mwana kuwa rais badala ya baba.

Katika uchaguzi wa kitaifa wa tarehe 30 Julai 2006 alipata kura nyingi kuliko wagombea wote kuwa rais lakini hakufikia nusu ya kura zote. Katika uchaguzi wa pili kati yake na Jean-Pierre Bemba alishinda akathibitishwa kuwa rais tarehe 17 Novemba 2006. Joseph Kabila ni rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyechaguliwa na wananchi wote katika uchaguzi huru.

Maisha yake

[hariri | hariri chanzo]

Joseph Kabila alizaliwa mjini Hewa Bora katika mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa Kongo. Baba yake alikuwa mwanasiasa na kiongozi wa kikundi cha wanamgambo waasi waliopinga serikali ya Mobutu Sese Seko.

Pamoja na familia ya baba Joseph alihamia Dar es Salaam (Tanzania. Alisoma shule ya msingi na ya sekondari huko Dar es Salaam na shule ya sekondari Sangu secondary (Mbeya). Anasemekana wakati ule alitumia jina la Hippolyte Kanambe Kazemberembe Kabange Mtwale kwa sababu za usalama.

Mwaka 1996 alijiunga na wanamgambo wa baba yake katika vita vya Kongo ya Mashariki.

Baada ya ushindi wa wapinzani dhidi ya Mobutu, baba alikuwa rais na Joseph alipelekwa masomoni kwenye chuo cha kijeshi huko Uchina. Wakati wa kurudi alipewa cheo cha jenerali jeshini na mwaka 2000 alipandishwa cheo kuwa mkuu wa jeshi.

Tangu kuwa rais mwaka 2001 Joseph Kabila alijitahidi kumaliza hali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Kongo akakubali kufika kwa walinzi wa amani wa UM.

Mnamo Desemba 2002 alikubali mapatano ya amani kati ya serikali na waasi yaliyokuwa msingi wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa na maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2006.

Katika Juni 2006 alimwoa Olive Lembe di Sita aliyekuwa mchumba wake wa miaka mingi na mama wa binti aliyezaliwa mwaka 2001.

Mnamo Oktoba 2021, Joseph Kabila alitetea tasnifu yake ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Johannesburg. Shahada ya uzamili katika sayansi ya siasa na uhusiano wa kimataifa alitunukiwa mwishoni mwa masomo yake ambayo yalidumu kwa miaka mitano.

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Joseph Kabila kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.