[go: up one dir, main page]

Uvutano

(Elekezwa kutoka Mvutano)

Uvutano (pia: mvutano, kani ya mvutano, kanimvutano, nguvu ya uvutano, nguvu mvutano na graviti, kutoka Kiingereza: gravity) ni kani ya kuvutana iliyopo kati ya maada yote ya ulimwengu. Kila gimba lenye tungamo linavuta magimba mengine yote yenye tungamo.

Taswira ya kani ya uvutano.
Mwendo wa maji yanayotoka kwenye nozeli kuelekea juu unabadilishwa mwelekeo wake kwa umbo la parabola kutokana na kani ya uvutano ya dunia.

Ndiyo sababu watu wanatembea ardhini ilhali hawawezi kuelea hewani: kwa sababu tungamo ya Dunia inawavuta kuelekea kiini chake. Inavuta kila kitu chenye tungamo kuelekea kiini chake. Sisi watu pia tunaivuta Dunia, lakini kani hiyo ni ndogo mno kulingana na tungamo kubwa ya Dunia. Dunia yetu imeshikwa na uvutano mkali wa Jua na ndiyo sababu ya Dunia kubaki karibu na Jua katika njiamzingo isiweze kwenda mbali.

Uvutano ni kani isiyo na kikomo lakini athira yake inapungua kadiri magimba yalivyo mbali. Unasababisha maada ya anga-nje kupangwa kwa nyota, nebula, majarra na makundi ya majarra.

Isaac Newton anajulikana kama mtaalamu aliyeweza kueleza uvutano kwa mara ya kwanza kama utaratibu wa msingi wa sayansi.

Mifano ya athira ya uvutano

hariri

Jiwe likitupwa hewani, litaanguka chini. Hii ni kwa sababu, ingawa kani ya mkono ilipeleka jiwe kwenda juu, kani ya uvutano ya Dunia inapunguza kasi ya jiwe na hatimaye inalirudisha ardhini.

Tabia ya kuvutana inaonekana vyema kati ya Dunia na Mwezi. Dunia ni kubwa, inauvuta Mwezi na kuushika kwenye njia yake ya kuzunguka Dunia. Lakini wakati huohuo Mwezi unavuta pia Dunia na hii inaonekana baharini katika mabadiliko ya maji kupwa na maji kujaa kila siku. Maji ya bahari huvutwa na Mwezi kiasi kwamba kwenye sehemu ya Dunia inayotazama Mwezi, maji ya bahari yaliyo moja kwa moja chini ya Mwezi huinuliwa kiasi cha nusu mita juu ya wastani wa usawa wa bahari yote.

  Makala hii kuhusu mambo ya fizikia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Uvutano kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.