[go: up one dir, main page]

Nenda kwa yaliyomo

Moctezuma II

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Moctezuma II alivyochorwa na Mhispania Antonio Rodriguez (1636-1691).
Moctezuma II katika Codex Mendoza, picha iliyochorwa na Azteki

 

Moctezuma Xocoyotsin (kwa Kinahuatl Motekusoma, kwa Kiingereza mara nyingi Montezuma, akirejelewa katika vyanzo vya Kihispania kama Moctezuma II; 1466 hivi - 29 Juni 1520) alikuwa mfalme wa tisa wa Tenochtitlan na mfalme mkuu wa sita wa Milki ya Azteki.[1] Alitawala kuanzia mwaka 1502 au 1503 hadi 1520.

Mawasiliano ya kwanza kati ya staarabu za kiasili za Meksiko na Wazungu yalitokea wakati wa utawala wake. Aliuawa katika mapigano kati ya Wahispania na Waazteki, wakati kiongozi wa Wahispania, conquistador Hernándo Cortés na watu wake walipigana naye kutwaa mji mkuu Tenochtitlan.

Wakati wa utawala wa Moctezuma II, Milki ya Azteki ilifikia upanuzi wake mkubwa zaidi. Kwa njia ya vita Moctezuma alipanua eneo upande wa kusini hadi Chiapas na shingo ya nchi ya Tehuantepec. Alivamia pia Wazapoteki na Wayopi na kuwaingiza katika milki yake[2].

Mnamo mwaka 1518, [3] Moctezuma alipokea taarifa za kwanza za Wazungu kutua kwenye pwani ya mashariki ya milki yake. Moctezuma aliamuru afahamishwe kuhusu matukio mapya ya wageni kwenye pwani na kuweka walinzi wa ziada na minara ili kukamilisha hilo.

Wakati Cortés alipofika mwaka 1519, Moctezuma alifahamishwa mara moja akatuma wajumbe kukutana na wageni; akatuma zawadi kwa Wahispania, pengine ili kuwaonyesha ubora wake.

Tarehe 8 Novemba 1519, Moctezuma alikutana na Cortés kwenye barabara kuu inayoelekea Tenochtitlán na viongozi hao wawili walibadilishana zawadi. Moctezuma alimpa Cortés zawadi ya kalenda ya Waazteki, diski moja ya dhahabu iliyobuniwa na nyingine ya fedha. Baadaye Cortés aliyayeyusha haya kwa thamani yao ya kifedha.

Siku sita baada ya kuwasili kwa Wahispania mjini Tenochtitlan, walimkamata mfalme na kumweka chini ya ulinzi kwenye 14 Novemba 1519.

Inasemekana kwamba Waazteki walizidi kuchukizwa na jeshi la Wahispania kukaa Tenochtitlán, na Moctezuma alimwambia Cortés kwamba ingekuwa bora kama wangeondoka. Baada ya shambulio la Wahispania dhidi ya mkutano wa wakubwa wa Azteki, mapigano yalianza na wananchi walishambulia Wahispania kwa nguvu zote.

Katika mapigano hayo Moctezuma aliuawa kwenye tarehe 30 Juni 1520. Taarifa mbalimbali zinapishana, haieleweki kama aliuawa na Waazteki au na Wahispania.

Wahispania walilazimika kukimbia mji. [4]

Moctezuma alifuatwa na mdogo wake Cuitláhuac, ambaye alikufa muda mfupi baadaye wakati wa janga la ndui. Alifuatwa na mpwa wake kijana, Cuauhtémoc [5]. Wakati wa kuzingirwa kwa jiji hilo, wana wa Moctezuma waliuawa na Waazteki, labda kwa sababu walitaka kujisalimisha. Kufikia mwaka uliofuata, Milki ya Azteki ilikuwa imeanguka kwa jeshi la Wahispania na washirika wao wenyeji, hasa kutoka mji wa Tlaxcala, ambao walikuwa maadui wa jadi wa Waazteki.

  1. "Aztec Political Structure". Tarlton Law Library. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2023-01-11. Iliwekwa mnamo 10 Machi 2020.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. https://archive.org/details/aztecwarfareimpe0000hass Hassig, Ross (1988). Aztec warfare: imperial expansion and political control. Norman: University of Oklahoma Press. ISBN 9780806121215. OCLC 17106411.
  3. Anales de Tlatelolco [Annals of Tlatelolco] (kwa Kihispania na Nahuatl). Ilitafsiriwa na Tena, Rafael. México, D.F.: Conaculta. 2004 [1528]. uk. 99. ISBN 970-35-0507-4.
  4. Nardo, Don (2009). The Spanish Conquistadors. Lucent Books. uk. 57.
  5. Paul Gillingham, Cuauhtemoc's Bones: Forging National Identity in Modern Mexico. Albuquerque: University of New Mexico Press 2011, uk 11.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]