Ufukara wa hiari
Ufukara wa hiari ni hali ya maisha ambayo baadhi ya watu wanaichagua kwa sababu za kifalsafa, za kimaadili na hasa za kidini. Katika Ukristo ni maarufu hasa Antoni abati na Fransisko wa Asizi.
Thamani ya ufukara huo inaeleweka kwa kuzingatia fujo zinazotokana na tamaa ya vitu, uchu wa mali, choyo, ubepari na usahaulifu wa njaa inayoua mafukara. “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha” (1Tim 6:10). “Kinyume cha mema ya Kiroho, malimwengu yanatenganisha watu, kwa kuwa hayawezi kuwa ya wengi kwa mkupuo moja na kikamilifu” (Augustino). Hivyo utafutaji wake usiporatibiwa unatenganisha, wakati utafutaji wa mema ya Kiroho unaunganisha watu. Kwa mfano, Mungu tunaye kadiri tunavyomshirikisha kwa wenzetu, kumbe tukiwanyima tunakuja kumkosa.
Katika Ukristo
haririUkamilifu wa Kikristo unategemea hasa upendo, lakini tukitaka kuufikia ni lazima walau tuwe na roho ya mashauri ya Kiinjili, kama Yesu alivyohimiza wote kuwa nayo aliposema, “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao” (Math 5:3): kwa namna fulani ni wao tangu sasa, si baadaye tu. Maana yake ni kwamba tusiambatane na malimwengu kwa kuwa: “Muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana; na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu. Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita” (1Kor 7:29-31).
Roho ya kutoambatana na malimwengu inahitajika pia ili tuelewe maana halisi ya haki ya kumiliki ambayo ni haki ya kujipatia na kusimamia vitu, ila “kuhusu kuvitumia mtu hatakiwi kuviona kama ni vyake, bali vya pamoja, awashirikishe wengine kwa urahisi katika shida zao” (Thoma wa Akwino). “Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha. Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo; huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli” (1Tim 6:17-19).
Roho hiyo inatukumbusha kwamba katika shida kubwa fukara akiomba chakula na kukataliwa anaweza kujichukulia bila kutenda dhambi ya wizi. Hiyo ni kweli vilevile kuhusu nyumba na nguo za lazima. Ni amri tutoe ziada yetu ili kumsaidia mwenye shida kubwa. Turudie ufukara wa Kiinjili ili kupinga maonevu ya ubepari yanayomkatisha tamaa asiye na kazi, anayeshindwa kulisha watoto wake. “Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali” (Zab 10:2). Tajiri, badala ya kuwa mlimbikizaji, anapaswa kuwa msimamizi wa riziki za Mungu kusudi fukara wapate mahitaji yao. Hapo haishi tena chini ya utawala wa uroho na kijicho, bali katika utawala wa Mungu. Vurugu na hatari kubwa za jamii ya leo zinatulazimisha tuzingatie na kutekeleza kweli hizo tusishikamane na vitu.
Thamani ya roho hiyo inatuelea zaidi tukikumbuka mema halisi tunayopaswa kuyatamani: “Msisumbukie maisha yenu, mle nini na mnywe nini, wala miili yenu, mvae nini. Maisha je, si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je, si bora kupita hao?… Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho, kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe” (Math 6:25-26,33-34). Roho hiyo inatuelekeza tutamani zaidi mema ya milele na kutegemea misaada ya Mungu ili kuyafikia. Ufukara wa hiari na tumaini kwa Mungu vinaongozana: kadiri tunavyoacha kuambatana na dunia tunatamani mema ya mbinguni, na kadiri tusivyotegemea misaada ya kibinadamu tunategemea ile ya Mungu. Kwa hiyo tumaini ndiyo roho ya ufukara ambayo kila Mkristo anapaswa kuwa nayo.
Yesu, aliyefanya utume wake akikosa hata makao (Math 8:20), alimhimiza tajiri aliyemkimbilia: “Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate” (Mk 10:21). Utekelezaji wa vitendo wa ufukara huo ni shauri, si amri; lakini kila mtu awe walau na roho ya shauri hilo: “Ukiwapenda mafukara, uende mara nyingi kati yao; ufurahi kuwaona nyumbani pako na kuwatembelea; uongee nao kwa radhi na kufurahi kuona wakikukaribia… Ukitaka kufanya zaidi, ujifanye mtumishi wa mafukara, ukienda kuwauguza wakiwa wagonjwa… ukiwahudumia kwa gharama yako… Mtakatifu Ludoviko IX mara nyingi aliwahudumia mezani mafukara aliowategemeza, na karibu kila siku aliwakaribisha watatu mezani pake; mara nyingi alikula mabaki ya supu yao kwa upendo usio na kifani… Yatakapokupata majanga yatakayokufanya uwe fukara… moto, mafuriko, kesi… ndio wakati hasa wa kutekeleza ufukara… kwa upole na uvumilivu” (Fransisko wa Sales). Ufukara wa Kikristo unatakiwa kuwa mfurahivu, na aliyeuchagua anapaswa kuvumilia walau tabu fulani kwa upendo wa Mungu, la sivyo utawezaje kumuunganisha naye? Fransisko wa Asizi na wengineo wametuonyesha linavyoweza kutufikisha kwenye muungano wa dhati na Mungu.
Matunda ya ufukara wa hiari
haririYesu alichagua ufukara kwa sababu nne zinazofanya ulete mara mia zaidi kadiri ya ahadi yake: 1) asisumbukie malimwengu; 2) aonyeshe kuwa anatafuta wokovu wa watu tu; 3) ahimize kutamani mema ya milele; 4) uwezo wa Mungu wa kuokoa uonekane wazi katika utovu wa misaada ya kibinadamu.
Kwanza, roho ya ufukara inatukomboa tusihangaikie vitu, ambavyo hapo si tena vizuio katika kumuendea Mungu, bali vyombo vya kutendea mema. Hapo tunaweza kupiga mbio kwenye njia ya ukamilifu kwa kuwa hatulemewi na mizigo isiyo ya lazima: hatufikirii tena kukaa duniani kana kwamba ni makao ya milele, bali tunajielewa kuwa wapitanjia tu na tunatamani kufikia lengo kuu pasipo kuchelewa.
Pili, ufukara wa hiari ni ishara ya kutojitafutia faida; ishara hiyo inahitajiwa na mtume ili kila mtu amuone nia yake pekee ni kumpatia Bwana watu.
Tatu, ufukara wa hiari unazaa katika jamii kwa namna ya ajabu: ili tujihakikishie inatosha kutembelea nyumba za kuwahudumia maskini zinazotegemea tu misaada inayopatikana siku kwa siku; ni kama muujiza wa kudumu unaofanywa na Mungu kwa kuitikia imani ya mwanzilishi na ya wanae.
Nne, roho ya ufukara inazaa matunda ya Kiroho ya ajabu zaidi tena: inatufundisha subira, unyenyekevu, kutoambatana na yale yote ambayo si Mungu wala upendo wake, yaani kutoambatana na mema ya akili, mema ya moyo na mema kadhaa ya roho. Mema ya akili ndiyo ujuzi wetu: tunaposoma tunapaswa kukwepa udadisi, majivuno na juhudi za kibinadamu tu, ili tusome kwa kumtumikia Mungu, tukijibandua na mitazamo yetu. Hapo Bwana atatujalia mara mia hata katika hayo: yaani atatujalia ule unyofu wa hali ya juu unaohitajika kwa sala ya kumiminiwa kwa kuwa unajisahau ili kuzama katika kuzingatia ukweli. Mema ya moyo ndiyo mapendo yetu na yale wanayotupatia wengine huku yamejaa heshima na imani kwetu. Ili tusitumbukie maisha ya miguso tu, inatubidi tusitamani kupendwa na kuheshimiwa, bali tumtolee Mungu hata mapendo halali yawe chini ya upendo halisi, ambao utatuonyesha thamani ya urafiki mkarimu usio wa kibinadamu tu. Huo ni zawadi kubwa ambayo pengine Mungu anawajalia walioachana na yote. Hatimaye kuna mema kadhaa ya roho ambayo ufukara unatufundisha kutoambatana nayo, yaani faraja za kihisi. Hatutakiwi kuzitafuta zisije zikawa kizuio badala ya msaada kwa kumuendea Mungu. Wengine wanajinyima pia mema yote yanayoweza kushirikishwa kutokana na sala na stahili zao, wakimuachia bikira Maria ayatumie kwa faida ya wenye shida kubwa zaidi duniani au toharani. Kwa kufanya hivyo wanajiandaa kupokea neema kubwa ya ufukara wa Kiroho wa juu zaidi unaopatikana katika utakaso wa mwisho, ule wa usiku wa roho unaokumbusha hali ya Yesu msalabani, alipojisikia mkiwa kupita kiasi.