Kalenda ya Gregori
Kalenda ya Gregori ni kalenda ambayo leo inatumiwa zaidi kimataifa. Jina limetokana na Papa Gregori XIII aliyeamua kutumia kalenda hiyo tangu tarehe 15 Februari 1582 badala ya Kalenda ya Juliasi.
Tabia za Kalenda ya Gregori
Kalenda inahesabu mwaka wa siku 365. Mwaka huo una miezi 12. Miaka inahesabiwa tangu "kuzaliwa kwake Kristo" kufuatana na makadirio ya Dionysius Exiguus. Siku hizi ni kawaida kuanzisha mwaka tarehe 1 Januari, lakini hayo ni mapatano ya baadaye, si utaratibu wa kalenda ya Gregori yenyewe.
Utaratibu wa wiki (au: juma) ya siku saba umeendelea: hauna uhusiano na utaratibu wa mwaka.
Miaka mirefu
Kalenda ya Gregori inashika vizuri muda wa mwaka wenyewe. Muda kamili wa mzunguko mmoja wa dunia kwenye mzingo wake ni siku 365.2425 kwa hiyo unazidi muda wa mizunguko 365 wa dunia kwenye kipenyo chake. Hivyo Kalenda ya Gregori inatumia utaratibu ufuatao wa kupatanisha tofauti hiyo:
- kila mwaka wa nne utakuwa na siku 366 badala ya 365 kwa kuongeza tarehe 29 Februari. Mifano: 1892, 1996; 2004, 2008, 2012
- kila mwaka ambao namba yake inagawiwa kwa 100 utakuwa na siku 365 (si 366 kwa sababu miaka hii inagawiwa kwa 4 pia!). Mifano: 1700, 1800, 1900, 2100
- kila mwaka ambao namba yake inagawiwa kwa 400 utakuwa tena na siku 366 (si 365 kwa sababu miaka hii inagawiwa kwa 100 pia!). Mifano: 1600, 2000, 2400, 2800
Sababu za matengenezo ya kalenda
Kasoro za Kalenda ya Juliasi
Papa Gregori XIII kama kiongozi wa kiroho wa dunia ya Kikatoliki (sehemu kubwa ya Ulaya) alitaka kusahihisha kasoro zilizoonekana katika kalenda ya awali. Tangu zamani za Waroma wa Kale hesabu ya wakati ilifuata Kalenda ya Juliasi iliyoanzishwa na Julius Caesar mwaka 46 KK. Kalenda hiyo ilikuwa na tatizo la kuwa urefu wa mwaka wake ulikadiriwa kuwa siku 365.25, kumbe ni siku 365.2425. Hivyo mwaka wa Juliasi ulipita muda kamili wa mwaka wa jua kwa dakika 11 na sekondi 14 yaani mwaka wa kalenda hii ulikuwa mrefu mno kiasi cha dakika 11 kila mwaka. Kosa lilikuwa dogo mwanzoni lakini lilizidi kuongezeka hadi hadi mwaka.
Kusogeza kwa tarehe ya Pasaka
Tatizo kwa maisha ya kanisa lilikuwa ya kwamba tarehe ya Pasaka iliendelea kusogea nyuma polepole na haikufuata tena utaratibu uliowekwa na mtaguso wa Nikea. Azimio hili katika mwaka 325 BK lilisema ya kwamba Pasaka itasheherekewa Jumapili ya kwanza baada ya mwezi mpevu wa kwanza baada ya 21 Machi (tarehe ya sikusare machipuo ambayo ni siku ya usawa wa mchana na usiku, hivyo mwanzo wa majira ya kuchipua katika kaskazini ya dunia). Wakati wa Papa Gregori XIII tarehe ya sikusare ilikuwa imewahi siku 10 na kufika tayari 11 Machi! Kwa sababu hiyo mtaguso wa Trento wa Kanisa Katoliki katika mwaka 1563 uliamua kusahihisha kalenda.
Dunia iliruka siku 10
Ni Papa Gregori XIII aliyeita wataalamu waliofanya makadirio mapya. Alifuata mapendekezo ya mtabibu Mwitalia Aloisius Lilius pamoja na padre na mwanahisabati Mjerumani Christopher Clavius.
Utaratibu wa mwaka mrefu (tazama juu) ulipokewa.
Pendekezo lingine lilikuwa namna ya kusahihisha kosa lililoingia tangu siku za kale. Wataalamu walipendekeza kufuta siku 10 ambazo tarehe ya sikusare machipua ilikuwa imesogea mbele.
Kosa lilinyoshwa kwa kufuta siku kati ya 4 Oktoba na 15 Oktoba mwaka 1582. Watu walikwenda kulala usingizi jioni ya 4 Oktoba 1582 wakaamka kesho yake tarehe 15 Oktoba 1582.
Kupokewa kwa kalenda mpya
Mwanzoni palikuwa na nchi chache tu zilizofuata kalenda mpya. Nje ya Italia zilifuata Hispania na Ureno katika Oktoba 1582, Ufaransa mwisho wa 1582.
Mengineyo ilikuwa suala la siasa kama nchi zilipokea utaratibu mpya haraka au la. Kwa jumla nchi za Kikatoliki ziliwahi kutumia kalenda mpya lakini nchi za Kiprotestanti zilichelewa kukubali: zilizo nyingi zikapokea kalenda mpya kuanzia mwaka 1700. Kwa karne nyingi kalenda hii ilikuwa jambo la Ulaya ya Magharibi tu lakini ilienea pamoja na ukoloni.
Nchi za Kiorthodoksi za Ulaya ya Mashariki zilikataa kalenda mpya hadi karne ya 20.
Nchi | Mwaka |
---|---|
Hispania na Ureno | 1582 |
Uholanzi wa kikatoliki | 1582 |
Ufaransa | 1582 |
Venezia (Italia) | 1582 |
Ujerumani wa Kikatoliki | tangu 1583 |
Uholanzi wa Kiprotestanti | 1700 |
Ujerumani wa Kiprotestanti | tangu 1700 |
Denmark | 1700 |
Uingereza pamoja na makoloni yake hivyo pia Marekani |
1752 |
Uswidi | 1753 |
Urusi | 1918 |
Ugiriki | 1924 |
Uturuki | 1926 |
Mahesabu ya kipindi cha badiliko kati ya kalenda mbili
Kwa jumla kipindi tangu kuanzishwa kwa kalenda hadi kupokewa katika nchi nyingi kilikuwa karibu miaka 300. Kipindi hiki cha kuwepo kwa kalenda mbili zilizofanana sana kinahitaji uangalifu mkubwa kwa upande wa wataalamu wa historia. Mara nyingi watu wa vijijini waliendelea kutumia hesabu ya zamani hata kama serikali kuu imeshatangaza matumizi ya kalenda ya Gregori. Hivyo hati mbalimbali zinaweza kutumia tarehe ambazo hazieleweki mara moja.
Mfano bora wa matatizo haya ni mapinduzi ya Urusi ya 1917. Chama cha Bolsheviki kilichukua utawala wa Urusi katika mchakato unaoendelea kuitwa "Mapinduzi ya Oktoba". Lakini sikukuu yake husheherekewa mwezi wa Novemba. Sababu yake ni kwamba mapinduzi yalitokea wakati kalenda ya kale bado ilikuwa kalenda rasmi ya Urusi ikatokea kwenye usiku wa 24/25 Oktoba 1917 kufuatana na kalenda ya Juliasi. Mwaka uliofuata 1918 Urusi ulijiunga na mfumo wa Kalenda ya Gregori. Kwa hiyo tarehe ya kumbukumbu ya mapinduzi ilisogezwa kufika mwezi wa Novemba.
Katika historia ya kipindi cha mabadiliko kuna maajabu kadhaa.
- Teresa wa Avila (mtakatifu wa Kanisa Katoliki) aliaga dunia mwaka 1582 katika usiku kati ya 4 Oktoba kwenda 15 Oktoba yaani katika usiku ambako Hispania ilibadilisha kalenda yake.
- Washairi Mwingereza William Shakespeare na Mhispania Miguel de Cervantes walikufa wote tarehe 23 Aprili 1616 ingawa Shakespeare alikufa siku 11 baada ya Cervantes - lakini mmoja alikufa nchini Hispania (iliyotumia tayari kalenda ya Gregori) na mwingine nchini Uingereza (bado ilifuata kalenda ya Juliasi)
Viungo vya nje
- Kibadilishi kalenda
- Inter Gravissimum (kwa Kilatini na Kifaransa pamoja na Kiingereza)
- maswali yaliyoulizwa mara kwa mara kuhusu kalenda
- kalenda ya Gregori kwa Kinorwei, ikiwa na taarifa kadhaa ya Norwei Archived 6 Oktoba 2014 at the Wayback Machine.
- Historia ya kalenda ya Gregori Archived 6 Januari 2014 at the Wayback Machine.
- Synoptical Julian - Gregorian calendar mlinganisho wa mfumo wa tarehe ya zamani na ya sasa 1582–2100.
- Kalenda ya Kudumu kutumika kwa mfumo wa tarehe za kalenda ya Gregori na nchi nyingi.